CHUO KIKUU KISHIRIKI CHA ASKOFU MKUU
YAKOBO
KITIVO
CHA SANAA NA SAYANSI ZA JAMII
IDARA
YA LUGHA, ISIMU NA FASIHI
JINA LA
KOZI: FASIHI LINGANISHI YA KISWAHILI
JINA LA
MHADHIRI: MIGODELA, W.
AINA YA
KAZI: KAZI
YA KIKUNDI
KUNDI
NAMBA: 2
WASHIRIKI
S/N.
|
JINA
|
NAMBA YA USAJILI
|
SAHIHI
|
01.
|
CYPRIAN
SIMEO, S
|
45289
|
|
02.
|
KANANI
EUGENIA
|
45325
|
|
03
|
KWILASA
DANIEL
|
45343
|
|
04.
|
MWAIPONJ
A ANNE
|
45387
|
|
05.
|
MWAKYANDO
SAMWEL
|
45391
|
|
06.
|
PONERA
JESKA, L
|
45428
|
|
07.
|
TAMIMU
RAJABU, A.
|
45447
|
|
08.
|
MUNG’ONG’O
WITNESS
|
45466
|
|
09.
|
MBIJIMA
VICTOR
|
45506
|
SWALI;
Mchango
wa Tafsiri katika Fasihi ya Kiswahili.
Utangulizi
Dhana ya Tafsiri na Fasihi Linganishi kwa mujibu wa
wataalamu mbalimbali.
Mwansoko na wenzake (2006) wanafasili Tafsiri kuwa ni zoezi
la uhawilishaji wa mawazo katika maandishi kutoka lugha moja hadi nyingine.
As-safi akimnukuu Dubois (1974) anaeleza kuwa Tafsiri ni
uelezaji katika lugha nyingine au lugha lengwa wa kile kilichoelezwa katika
lugha nyingine (lugha chanzi) ikihifadhi maana na mtindo wa matini chanzi.
Catford (1965:20) anasema tafsiri ni kuchukua mawazo yaliyo
katika maandishi kutoka lugha moja (lugha chanzi) na kuweka badala yake mawazo
yanayolingana katika lugha nyingine (lugha lengwa).
Boldor (2003) akimrejelea Compbell (1926) Fasihi Linganishi ni
taaluma inayochunguza uhusianao uliopo baina ya fasihi mbili au zaidi nje ya
mipaka ya kitaifa kwa njia ya kulinganisha mfanano na msigano
Henry Remak (1971) anafasili Fasihi Linganishi kama uwanja
wa kifasihi unaohusika na uchunguzi na mahusianao ya kifasihi nje ya mipaka ya
nchi moja, pia kati ya fasihi na fani nyinginezo. Kwa maelezo haya ya Remak
tunachoweza kusema ni kwamba Fasihi Linganishi haiishii kuangalia mahusino ya
kifasihi peke yake bali huangalia mahusiano kati ya fasihi na fani nyinginezo
zisizo za kifasihi.
Wamitila (2003) anaeleza kuwa fasihi linganishi inahusu uchambuzi wa maandishi ya wakati
mmoja na aina moja na katika lugha mbalimbali kwa nia ya kumiliki sifa zinazoyahusisha kama athari, vyanzo, sifa zinazofanana na
tofauti za kiutamaduni. Anaendelea kueleza kuwa inawezekana kufanya hivi kwa
nia ya kuangalia matapo mbalimbali, maendeleo au hata nadharia za kiuhakiki.
Fasihi ya namna hii iliweka misingi na juhudi za wanaisimu kuanza kuilinganisha
lugha mbalimbali katika karne ya kumi na tisa.
Kutokana na fasili zote hizo kuhusu tafsiri tunaweza
kuhitimisha kwa kusema kuwa, tafsiri ni uhawilishaji wa mawazo, ujumbe au
taarifa iliyopo katika maandishi kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa bila
kupoteza maana ya msingi na mtindo uliotumika katika matini chanzi. Na maana
katika tafsiri inatakiwa iendane na lengo la mtunzi wa matini chanzi lakini pia
kwa kuzingatia utamaduni wa jamii unayoitafsiriya.
Pia Fasihi Linganishi ni aina ya fasihi ambayo inajikita
zaidi kutumia mbinu za kiulinganishi baina ya kazi mbili za kifasihi ili kujua
sifa fulani fulani kama vile kufanana kwa kazi hizo, tofauti za kiutamaduni
katika kazi hizo, kujua ulinganishi katika lugha yaani sarufi ya lugha katika
kazi hizo za kifasihi.
Historia
na Maendeleo ya Tafsiri nchini Tanzania.
Wanjala (2011) anaeleza kuwa, historia ya tafsiri
imeangaliwa kwa kuegemea vipindi muhimu vya maendeleo na mabadiliko ya elimu na
utamaduni. Nchini Tanzania, tafsiri haina historia ndefu sana kwani imeanzia mnamo
karne ya 19 na inaweza kugaiwa katika vipindi vitatu vikuu navyo ni kabla ya
utawala wa kikoloni, wakati wa utawala wa kikoloni na baada ya uhuru.
Kabla
ya utawala wa kikoloni
Kabla ya utawala wa kikoloni wamishionari walitafsiri vitabu
mbalimbali vya kikristo ikiwemo Biblia Takatifu kutoka lugha ya Kiingereza
kwenda Kiswahili na lugha nyingine za makabila kwa lengo la kueneza dini na
ustaarabu wa kikristo kwa waafrika.
Kipindi
cha Ukoloni
Hiki ni kipindi kuanzia miaka ya 1800, katika kipindi hiki,
wakoloni hasa waingereza walitafsiri maandiko mbalimbali ya kitaaluma na fasihi
ya Ulaya kwa lugha ya Kiswahili. Vile vile kabla ya uhuru zipo baadhi ya kazi
za fasihi zilizotafsiriwa na watanzania. Kwa mfano tamthiliya ya MZIMU WA WATU
WA KALE iliyotafsiriwa na Mohammed Said Abdalla (1960) kutoka lugha ya
kiingereza Shrine of The Ancestors.
Baada
ya Uhuru
Baada ya uhuru ambapo ni kuanzia mwaka 1961. Katika kipindi
hiki wapo wataalamu waliofanya juhudi za kutafsiri vitabu mbalimbali kwa lugha
ya Kiswahili. Mfano mzuri ni Mwalimu Julius K. Nyerere ambaye alitafsiri vitabu
viwili vya mwandishi mashuhuri wa Tamthiliya wa huko Uingereza aitwaye William
Shakespeare ambavyo ni tamthiliya ya JULIUS KAIZARI (Julius Caesar, 1963) na
tamthiliya ya MABEPARI WA VENIS (The Merchant of Venis, 1969). Kazi nyingine
zilizotafsiriwa baada ya uhuru ni WIMBO WA LAWINO (Song of Lawino)
iliyotafsiriwa na Paul Sozigwa (1975), riwaya ya UHURU WA WATUMWA (The Freeing
of the Slaves in East Africa) iliyotafsiriwa na East African Literature Bureau
(1967), NITAOLEWA NIKIPENDA (I Will Marry When I Want) iliyotafsiriwa na
Crement M. Kabugi (1982).
Kwa ujumla maendeleo ya taaluma ya tafsiri nchini Tanzania
yamepiga hatua kubwa kutokana na kukua kwa sayansi na teknolojia. Taaluma ya
tafsiri inafundishwa katika elimu ya sekondari na katika vyuo vikuu mbalimbali.
Pia taasisi na asasi zinazojishughulisha na tafsiri zimeongezeka kwa mfano
Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA), Taasisi ya Kiswahili na Lugha za
Kigeni (TAKILUKI) na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA).
Mchango
wa Tafsri katika Fasihi ya Kiswahili.
Tafsiri imesaidia katika kueneza dini na vipengele vingine
vya utamaduni kutoka mataifa ya nje. Tafsiri ni nyenzo ya kuenezea utamaduni kutoka
taifa moja kwenda jengine au kutoka jamii moja kwenda nyingine. Kwa mfano
kutokana na Wazungu kutafsiri Biblia na Waarabu kutafsiri Kur-An kwa lugha ya
Kiswahili, kulisababisha waafrika kwa ujumla kubadilisha dini zao za kijadi na
kufuata dini ya Ukristo na Uislamu.
Tafsiri imesaidia katika kukuza lugha na fasihi ya
Kiswahili. Lugha ya Kiswahili ni miongoni mwa vipengele muhimu sana katika utamaduni
wa Tanzania kwa sababu Kiswahili ni lugha rasmi, lugha ya taifa na Tunu ya
taifa. Kabla ya kuwepo taaluma ya Tafsiri, lugha ya Kiswahili ilionekana
kudumaa hasa katika nyanja ya sayansi na teknolojia. Lakini baada ya kuwepo
taaluma hii, wataalamu na Taasisi mbalimbali za Kiswahili zimekuwa zikifanya
jitihada za kutafsiri vitabu vya lugha mbalimbali kwenda lugha ya Kiswahili
pamoja na kutafuta Istilahi na Misamiati ya Kiswahili inayoweza kwenda sambamba
na Istilahi za Kisayansi. Mfano wa istilahi hizo ni kama vile Password –
Nywila, Keyboard – Kicharazio, Scanner – Mdaki, Flash Disc – Diski Mweko na
Mouse – Kiteuzi.
Tafsiri ilisaidia kuongeza hamasa ya usomaji wa kazi za
kifasihi. Historia inaeleza kuwa, wakati wa ukoloni fasihi ilidumaa kwa sababu Waafrika
hawakuwa na mwamko wa kusoma vitabu na kazi nyingi za kifasihi ziliandikwa kwa
lugha ya Kiingereza kwa lengo la kuwafurahisha Mabwana. Lakini baada ya
wataalamu wa fasihi kuanza kutafsiri kazi mbalimbali za fasihi ya Ulaya kwa
lugha ya Kiswahili na lugha nyingine za makabila mwamko wa kusoma vitabu
uliongezeka. Mfano wa vitabu vya fasihi vilivyotafsiriwa wakati wa ukoloni ni MZIMU
WA WATU WA KALE (Shrine of the Ancestors) iliyotafsiriwa na Mohammed Said
Abdalla (1960). Pia kuna kazi mbalimbali za kifasihi zilizotafsiriwa baada ya
uhuru, miongoni mwao ni Juliasi Kaizari (Julius Caesar) (1963) na MABEPARI WA
VENIS (The Merchant of Venis) (1967), zote hizo zimetafsiriwa na Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere. Baada ya hapo kazi mbalimbali za kifasihi kama vile hadithi
fupi, Riwaya, Tamthilia na Mashairi yalitafsiriwa kutoka lugha mbalimbali
kwenda katika lugha Kiswahili. Vile vile kazi za fasihi ya Tanzania zilitungwa
na kupelekea kukua na kuenea fasihi ya Kiswahili.
Tafsiri imesaidia katika kukuza elimu nchini Tanzania. Elimu
ikiwa ni sehemu ya utamaduni wa Tanzania, imepiga hatua kutokana na maendeleo
ya mitaala na mbinu mbalimbali za kufundishia. Tafsiri ni miongoni mwa mbinu
inayotumiwa na walimu wengi ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wanafikia lengo la
kujifunza kwa mujibu wa viwango vyao. Juhudi mbalimbali zinachukuliwa katika
kukuza elimu ya Tanzania. Miongoni mwa juhudi hizo ni kutafsiriwa kwa vitabu
vya masomo mbalimbali ili visaidie katika marejeleo. Vile vile taaluma ya
tafsiri imekuwa ni kozi muhimu katika shule za sekondari na vyuoni ili kuwapa
wanafunzi uwezo wa kuitumia taaluma hii ili waweze kujiajiri kwa kutafsiri kazi
mbalimbali.
Tafsiri imesaidia katika kuibua nadharia mpya ya Fasihi
Linganishi. Kama ijulikanavyo kuwa fasihi ni sanaa na sanaa ni sehemu ya
utamaduni. Kwa mujibu wa kitabu cha “Utangulizi wa Nadharia ya Fasihi
Linganishi” kilichoandikwa na Athumani S. Ponera (2014) ni kwamba, lengo la
nadharia hii ni kuchunguza kufanana na kutofautiana kati ya fasihi ya Tanzania
na fasihi ya mataifa mengine hasa Amerika na Ulaya na hata kazi za mwandishi
mmoja na mwandishi mwingine au kazi tofauti za mwandishi mmoja hususani katika
vipengele mbalimbali vya utamaduni pamoja na maendeleo ya sayansi na
teknolojia. Kwa hiyo kutokana na maelezo hayo ni wazi kuwa kuwepo kwa kazi
nyingi za mataifa ya nje zilizofasiriwa kwa lugha ya Kiswahili na zile ambazo
hazijafasiriwa ni sababu tosha iliyomsukuma mwandishi kuanzisha mjadala huu wa
nadharia mpya ya fasihi linganishi kama ilivyo kwa nadharia ya isimu
linganishi.
Tafsiri imesaidia katika kukuza biashara na kuinua uchumi wa
Taifa. Kama tulivyotangulia kusema
kuwa, utamaduni ni utu na utu ni muhimu katika maisha ya watu. Biashara ni
miongoni mwa sekta inayounganisha watu wa aina tofauti. Kuwepo kwa utu katika biashara ndio
kutasaidia kukuza biashara na uchumi wa nchi yetu. Mchango wa tafsiri katika
biashara ni kuwa mikataba mingi ya biashara na uwekezaji nchini Tanzania inatafsiriwa
kwa lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha wananchi kupata haki zao. Vile vile
matangazo mbalimbali ya kibiashara na taarifa nyingine katika vyombo vya habari
kama vile magazeti hutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ili kila mwananchi apate
kufaidika na huduma zinazotolewa.
Tafsiri imesaidia kuingiza utanzu mpya wa Fasihi Andishi
katika fasihi ya Kiswahili. Hapo
mwanzo kabla ya tafsri, Fasihi ya Kiswahili haikuwa na utanzu wa Tamthiliya
lakini kwa kutumia tafsiri hivi sasa Tamthiliya ni moja kati ya tanzu muhimu
katika Fasihi ya Kiswahili. Mifano ya Tamthiliya zilizo tafsiriwa ni pamoja na tamthiliya
ya JULIUS KAIZARI (Julius Caesar, 1963) na tamthiliya ya MABEPARI WA VENIS (The
Merchant of Venis, 1969), WIMBO WA LAWINO (Song of Lawino) iliyotafsiriwa na
Paul Sozigwa (1975), NITAOLEWA NIKIPENDA (I Will Marry When I Want)
iliyotafsiriwa na Crement M. Kabugi (1982).
Vilevile tafsiri imesaidia kueneza Fasihi ya Kiswahili na
utamaduni wake, kuna kazi za fasihi ya Kiswahili zilizotafsiriwa kwa lugha
nyingine za kigeni kwa mfano Riwaya ya Utengano imetafsiriwa kama Separazione
katika lugha ya Kiitaliano, hii inaashiria kuwa fasihi ya Kiswahili imeenea
hadi mataifa mengine.
Mchango
wa Tafsiri katika Fasihi Linganishi ya Kiswahili
Mbali na mchango wa Tafsiri katika Fasihi ya Kiswahili
lakini pia Tafsiri imekuwa na mchango mkubwa sana katika Fasihi Linganishi ya
Kiswahili, miongoni mwa mchango wa Tafsiri katika Fasihi Linganishi ya
Kiswahili ni pamoja na:
Tafsiri hutusaidia kujua na kuliganisha tamaduni za jamii
nyingine na ile iliyoandikiwa tafsiri. Kwa mfano katika Tamthilia ya NITAOLEWA
NIKIPENDA (I Will Marry When I Want) iliyo andikwa na Ngugi Wa Thiong’o na
kutafsiriwa na Crement M. Kabugi (1982). Tamthilia hii imetungwa katika
mazingira ya jamii ya Kikuyu, hivyo Tafsiri ya tamthilia hii imesaidia kujua
utamaduni wa Wakikuyu. Kwa mfano katika ukurasa wa 65, tunaweza kuona jinsi
ndoa ya Kikuyu inavyofungwa, utaratibu wa utoaji mahari pamoja na nyimbo
ziimbwazo wakati wa sherehe.
Pia kupitia Tafsiri tunaweza kujua historia ya jamii husika.
Katika Tafsiri ya Tamthilia ya NITAOLEWA NIKIPENDA tunaona historia ya Taifa la
Kenya tangu wakati wa ukoloni hadi wakati wa Uhuru. Kwa hiyo hapa tunaelewa
yale yote wananchi wa Kenya waliyoyapitia wakati wa Ukoloni, kwa mfano katika
uk. 32 mwandishi anaonesha adha walizopitia wananchi wa Kenya katika harakati
za kupigania uhuru na baadae wakafanikiwa, uk 33. Pia tunaona katika uk. 34
wananchi wanaingia katika kipindi kingine cha uhuru lakini bado wanaendelea
kupata adha zilezile kama walizozipata wakati wa Ukoloni.
Tafsiri husaidia kukuza Fasihi ya lugha lengwa. Kupitia Tafsiri,
Fasihi ya lugha lengwa inanufaika na kuingizwa vipengele kadhaa vya lugha
hususani misemo au methali ambazo hazikuwepo katika lugha lengwa, hivyo kwa
kutafsiri misemo hii lugha lengwa nayo pia itakuwa imenufaika na misemo hiyo. Kwa
mfano, msemo; “when axes are kept in a one basket they must necessarily knock
agaist each other” umefasiriwa kama;“vyuma vikiwa katika gunia moja havikosi
kugongana” uk. 24. Kwa hiyo tunaweza kuwa tumeongeza msemo mwingine katika
Kiswahili kupitia Tafsiri hii.
Vilevile tafsiri imeongeza idadi ya machapisho ya vitabu vya
Fasihi ya Kiswahili na hivyo itakuwa imeimarisha na kukuza fasihi ya Kiswahili
nchini Tanzania. Mfano; tamthiliya ya JULIASI KAIZARI (Julius Caesar) (1963) na
tamthiliya ya MABEPARI WA VENIS (The Merchant of Venis) (1969) iliyotafsiriwa
na Mwalimu Julius K. Nyerere, WIMBO WA LAWINO (Song of Lawino) iliyotafsiriwa na
Paul Sozigwa (1975), riwaya ya UHURU WA WATUMWA (The Freeing of the Slaves in
East Africa) iliyotafsiriwa na East African Literature Bureau (1967), NITAOLEWA
NIKIPENDA (I Will Marry When I Want) iliyotafsiriwa na Crement M. Kabugi
(1982), Riwaya ya BARUA NDEFU KAMA HII iliyoandikwa na Mariama Bâ katika lugha
ya kifaransa (Une si longue lettre) ikatafsiriwa katika lugha ya Kiingereza na Kiswahili
na Professor Maganga.
Pia tafsiri hutusaidia kujua itikadi ya mwandishi na pengine
itikadi ya jamii husika. Kwa muktadha wa tamthilia ya Nitaolewa Nikipenda
tunaona mwandishi anapinga sana tamaduni na
mtindo wa maisha ya kimagharibi ikiwa ni pamoja na dini za kigeni, lugha
zao na mambo yote yaliyoletwa na Wakoloni mfano katika ukurasa wa tano (uk 5).
Kama unahitaji huduma ya kuandikiwa makala katika tovuti yako, au huduma yoyote basi wasiliana nami kupitia:-
SIMU: +255 755 987 604, +255 789 198 345
E-MAIL: reubentanzania@gmail.com
Hitimisho
Katika kazi hii tumeangalia vitabu vya Fasihi ya Kiswahili
vilivyotafsiriwa, tumeangalia mchango wa Tafsiri katika Fasihi ya Kiswahili na
kugusia kwa uchache mchango wa tafsiri katika Fasihi Linganishi. Kwa hiyo
kulingana na kazi hii tunaweza kuona mchango na nafasi ya tafsiri katika
taaluma ya Fasihi ya Kiswahili, hivyo kuna ulazima mkubwa kwa mtu
anayeshughulika na Tafsiri awe ni mjuzi wa Fasihi, hii ni kwa lengo la
kuzalisha zao bora la Tafsiri ya Kifasihi. Lakini pia kuna ulazima mkubwa kwa
mtaalamu wa Fasihi Linganishi kujua taaluma ya Tafsiri kwa sababu anapofanya
ulinganishi kati ya tafsiri na kazi za kifasihi ni lazima uwe na uelewa wa
kutosha juu ya taaluma ya Tafsri. Kwa hiyo Fasihi Linganishi na Tafsiri
kimsingi ni taaluma zinazoshikamana kuliko kuachana.
MAREJELEO
Mwansoko, H.J.M na wenzake (2006) .Kitangulizi cha Tafsiri,
Nadharia na Mbinu. TUKI. Dar-es-salaam
Remak, H.H. (1971). Comperative literature: Its Definition and
Function. Carbondale: Southern Illinois.
Wamitila, K. W. (2003) Kamusi ya Fasihi: Istilahi na
Nadharia. Nairobi: Focus Publication
Wa Thiong’o, N. & Wa Mirii (1982). I Will Marry When I
Want. East African Educatinal Publishers: Nairobi.
Wa Thiong’o, N. & Wa Mirii (1982). Nitaolewa Nikipenda.
East African Educatinal Publishers: Nairobi.