MKONDO WA KIMAREKANI KATIKA
FASIHI LINGANISHI
Tangu Marekani ilivyoanza kujiingiza katika fasihi
linganishi, huonesha kwa nguvu kuwepo kwa mipaka iliyopo katika mkondo wa
kifaransa. Walipenda kuendeleza fasihi linganishi kwa kuikuza kwa maneno
mbalimbali katika sanaa na fasihi kwa ujumla, kukua na kujifunza ulinganishi
katika nchi ya marekani. Vilevile kulikuwa na mawazo ya waasisi katika chuo
kikuu cha Marekani, walifungua dirisha la kuzalisha fasihi iliyoambatana na
muunganiko wa mawazo tofautitofauti tangu mwanzo wa historia ya marekani.
Maendeleo ya nadharia ya fasihi linganishi yaliendana
sambamba na mawazo ya waasisi kama vile Henry Remark na Rene Wellek.
Mwanzilishi wa shule ya kimarekani aliyejitokeza katika nusu ya karne ya 20
alikuwa ni Henry Remark. Mwasisi huyu anasema fasihi linganishi huwa
haifungamani na taaluma inayojitegemea bali huwa na mwingiliano kati ya taaluma
moja au sehemu husika. Vilevile anaendelea kueleza kuwa ulinganifu huwa
unajitokeza kati ya fasihi mbili au zaidi tofauti na kazi ya fasihi na taaluma
nyingine kama vile muziki, uchoraji, falsafa, utaalamu wa ujenzi wa nyumba,
dini, saikolojia, hesabu, fizikia na kemia.
Mtazamo huu ulikuwa tofauti na mkondo wa kifaransa. Mkondo
huu ni wa kimapinduzi kwa vile walilenga kukosoa mitazamo ya kifaransa na
kijerumani. Kasoro kubwa waliyoiona ni kuegemea katika misingi ya kinadharia
katika kutazama na kuchanganua masuala ya kisanaa.
Waasisi wa mkondo wa kimarekani Henry Remak, Robert Clement
na Rene Welleck wamekuwa na mawazo juu ya nadharia hii kama ifuatavyo;
Kwa mujibu wa Henry Remak ambaye anatambulika kama baba wa
mkondo wa kimarekani mwaka 1971 yeye alisema, fasihi linganishi kama uwanja wa
kifasihi unao husika na uchunguzi na mahusiano ya kifasihi nje ya mipaka ya
nchi moja, pia kati ya fasihi na fani nyinginezo.
Remak akaja na mawazo ya kuwepo kwa fasihi linganisi na
fasihi ya kitaifa, hakuna utofauti kati ya fasihi linganishi na fasihi ya
kitaifa, kutokana na kuwa fasihi linganishi ni fasihi inayo jishugulisha na nje
ya mipaka pia fasihi ya kitaifa ni fasihi ambayo huwa na mfanano sana katika
tafsiri husika ya fasihi.
Pia anaendelea kusema wazo lingine la uwepo wa fasihi
linganishi na fasihi jumla, kuna utofauti kati ya fasihi linganishi na fasihi
jumla. Fasihi linganishi hujumuisha elementi ya eneo, muda, aina na watu. Katika jografia hujumuisha fasihi jumla,
ambayo huwa na vipengele vyake kama vile eneo. Pia hujishughulisha na uhusiano
kati ya nchi mbili au waandishi wawili katika nchi tofauti au mwandishi mmoja
katika kazi zake tofauti.
Hivyo kwa maelezo haya ya Remak tunaweza kusema kwamba
fasihi linganishi haiishii kuangalia mahusiano ya kifasihi peke yake bali
huangalia mahusiano kati ya fasihi na fani nyingine zisizo za kifasihi. Fasihi
linganishi isichukuliwe kama taaluma pekee bali kama kiunganishi baina ya
masomo au kama sehemu ya somo.
Rene Wellek, katika kitabu chake cha ``Theory of Literature’’ ambacho pia kiliweza kutafasiliwa kwa lugha
ya kiarabu na Sharif Al Sayed (1989) alieleza yafuatayo;
Neno fasihi linganishi kama linavyochukuliwa na shule ya
kifaransa ni dhana nzito na yenye kuchanganya katika Nyanja mbalimbali za
kuichambua fasihi, hivyo basi jitihada za kupata ujuzi katika shule ya
kifaransa juu ya fasihi linganishi ilikuwa duni.
Welleck yeye alipinga uwepo wa mipaka katika kuiangalia
fasihi, kwa upande wake anasisitiza kuwa katika kuiangalia fasihi linganishi ni
vyema kuihusisha na historia ya fasihi, fasihi ya kitaifa na fasihi jumla. Anaendelea
kusema kuwa fasihi linganishi inakusudia
kuondoa fikra au hisia za utaifa na mtazamo finyu lakini haidharau uwepo wa
tamaduni tofauti za mataifa na kukua kwake na wala haikusudii kupunguza au
kuondoa umuhimu wake lakini tunatakiwa kuwa makini na machaguo yasiyo sahihi
ambayo hayaitajiki kwasababu twahitaji vyote yaani fasihi ya kitaifa na fasihi
ya kiujumla.
Misingi ya Mkondo wa
Kimarekani katika Fasihi Linganishi.
(i). Fasihi linganishi lazima iambae katika nyanja zingine
za kitaaluma na maisha kwa ujumla kama vile historia, muziki, saikolojia dini
na tamaduni za jamii nyingine.
(ii). Mipaka ya fasihi linganishi lazima iwe huru kutoka
taifa moja na taifa lingine kwa sababu fasihi linganishi inahusisha fasihi
mbili au zaidi ni lazima ichangie na kuhimiza mahusiano ya kitaaluma kutoka
mipaka ya taifa moja hadi taifa lingine. Remak anasema, pamoja na tofauti za
kilugha na kiutamaduni mataifa yote hufanana kwa baadhi ya vitu.
(iii). Fasihi Linaganishi yaweza kuwa na fasihi mbili au
zaidi. Kwa mujibu wa wataalamu hawa wanaona kuwa fasihi linganishi ni lazima
ilinganishe fasihi mbili au zaidi au fasihi mbili za mwandishi mmoja mfano
unaweza kufanya ulinganifu wa kazi za Kezilahabi, Penina Mlama na ibrahim
Hussein kwa pamoja. Lakini pia unaweza kufanya kazi ya kulinganisha kazi za
mwandishi mmoja kwa mfano, E.Kezilahabi “Rosamistika na dunia uwanja wa fujo”.
(iv). Lugha inayotakiwa hutumika katika fasihi Linganishi
yaweza kuwa lugha ya kikabila au ya kikanda ilimradi lugha hiyo iwe inatumika
katika lugha zote ambazo zaweza kuwa mbili au zaidi.
(v). Fasihi Linganishi hujikita katika kutumia mbinu za
kiuhalisia, kiutendaji na kiuhakiki kuhusu kufaa au kutofaa kwa sanaa za
ulimwengu. Fasihi ya kitaifa haitengwi na fasihi jumla. Fasihi Linganishi haina
maana au haitastawi kama itawekewa mipaka na kuwa taaluma ya fasihi peke yake
Nyanja za Kiuchunguzi.
- Usambamba
Hii inakwenda tofauti na taathira ya wafaransa, uwanja huu
unaonesha kuwa kuna kufanana au kulingana kati ya fasihi za watu tofauti ambayo
mabadiliko yao ya kijamii yanafanana bila kujali kwamba kunakuathiriana kwa
karibu au kuna uhusiamo wa moja kwa moja.
Mfano mahusiano ya kisiasa na ya kijamii wakati wa ukabaila
yalipelekea kufanana kwa mkondo wa mawazo, sanaa na fasihi katika sehemu
mbalimbali za dunia.
Uwanja huu unaiangalia misingi inayoonyesha sifa za usanii
wa mwandishi na mwandishi, hauzingatii umuhimu wa kuhusianisha.
Haizipi umuhimu taathira, kuna uwezekano wa kuzishughulikia
matini za kifasihi bila kuonana/ kuwasiliana kwa aina yoyote bali kwa mazingira
au uhalisia unaofanana.
Kama taathira zipo katika matini za kifasihi umuhimu wake
haupo katika taathira yenyewe isipokuwa kwa mazingira. Kama mazingira
hayataruhusu tathira kuwa yenye tija bali taathira haitatokea
- Mwingiliano Matini
Maana ya mwingiliano matinni kwa mujibu wa Enani, ni
uhusiano kati ya matini mbili au zaidi katika kiwango ambacho kinaathiri
usomaji wa matini mpya. Matini inayoathiri inachanganywa na maudhui ya matini
inayo athiriwa, yaani kuathiriana kwa waandishi wawili.
Kwa mjibu wa Leon, S, Roudiz anasema ni mbadilishano wa
karibu wa mfumo wa ishara baina ya matini. Yaani ni kutumia mfumo mmoja wa uandishi
badala ya mwingine.
Hivyo basi wanasisitiza mwingiliano wa matini kwa kuwa kila
msomaji atachukua sehemu Fulani ambayo inaendana na utamaduni wake, lugha na
ujuzi kutoka katika matini. Yani:
-Matini mpya au ngeni inaingizwa kwenye matini ya zamani,
-Matini mpya inasomwa kwa kuzingatia matini ya zamani,
-Ni mchakato endelevu wa kuboresha matini ya zamani.
-Matini ya zamani inakuwa ni malighafi ya kutengeneza matini
mpya.
Ubora wa Mkondo wa
Kimarekani
(i). Walihusisha fasihi simulizi na fasihi andishi, mtazamo
huu ulijikita kuangalia fasihi kwa ujumla tofauti na mitazamo mingine kama vile
mtazamo wa kifaransa ambao ulijikita kuangalia fasihi andishi tu, mfano katika
fasihi simulizi walijikita kuangalia vipengele vya fasihi simulizi kama vile
muziki.
(ii). Mtazamo huu unaweza kufanya ulinganifu katika kazi
mbili ambazo zilitumia lugha moja kutoka mataifa mawili tofauti mfano kazi
iliyoandikwa kwa kiswahili nchini kenya ukilinganisha na kazi za kiswahili
nchini Tanzania mfano kazi ya Wamitila “bina-adam” na Kezilahabi “Nagona”. Hivyo
wamefanikiwa kutenganisha fasihi linganishi na suala zima la utaifa. Ambapo
mtazamo huu ulijikita katika mtazamo wa kimataifa.
(iv). Walitenganisha taaluma ya fasihi kutoka katika
vizingiti au vikwazo vya kisiasa, kitabaka na lugha.
(v). Wanasisitiza kuwa katika kufanya ulinganifu,
mlinganishaji asifungwe na njia moja ambapo wanadai kuwa njia ya kihistoria sio
njia pekee inayotumika katika kulinganisha kazi za kifasihi kutoka jamii au
mataifa tofauti.
Udhaifu wa Mkondo wa
Kimarekani
(i). Mkondo huu unachanganya fasihi na fani au taaluma
nyingine kama vile muziki, falsafa, saikolojia, uchoraji, hisabati na sayansi
ya jamii. Kama lilivyo jina la taaluma yenyewe yaani fasihi linganishi,
inaonyesha kuwa inahusika na ulinganishi wa kazi za kifasihi. Kuingiza taaluma
za falsafa, saikolojia hisabati au sayansi ya jamii katika fasihi linganishi ni
kuchanganya taaluma.
(ii). Mkondo huu unachanganya fasihi linganishi na fasihi
jumla kwa madai kwamba zote zinahusika na ujifunzaji wa somo moja yaani fasihi.
Lakini kiuhalisia, taaluma ya fasihi linganishi na fasihi jumla hazifanani
ingawa zote ni taaluma za fasihi. Fasihi linganishi inahusika na ulinganishi wa
kazi mbalimbali za fasihi lakini fasihi jumla haihusiki na ulinganishaji wa
kazi za kifasihi. Inaangalia kazi za fasihi kwa ujumla wake na umaarufu wa kazi
hizo duniani.
(iii). Usanii unatofautiana kutegemeana na taifa na
historia. Inategemea mambo ya kifasihi yanayozungumziwa na historia ya kila
jambo kama inafanana au siyo. Hii inatokana na mawazo yao katika uwanja wa
usambamba ambapo wanasema kuwa “kuna kufanana au kulingana kati ya fasihi za
watu tofauti ambao mabadiliko yao ya kijamii yanafanana bila kujali kwamba kuna
kuathiriana kwa karibu au kuna uhusiano wa moja kwa moja baina ya watu hao.”
Ukweli ni kwamba, jamii zinaweza kuwa zimepitia katika mfumo wa kijamii
unaofanana na jambo linalozungumziwa linaweza kuwa moja. Lakini, kama historia
ya jambo hilo inatofautiana kati ya taifa moja na taifa jingine, sanaa yake pia
itatofautiana.
(iv). Mkondo huu haukuzingatia suala la fasihi kuathiri au
kuathiriwa na kitu kingine wakati kiuhalisia fasihi inaweza kuathiri au
kuathiriwa na vitu kama vile utamaduni na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
(v). Kutumia fasihi ya Ulaya kama kielelezo cha fasihi jumla
ni udhaifu. Hii inatokana na jinsi Remak alivyoifasili fasihi jumla kuwa ni
“dhana inayotumika kuelezea machapisho ya fasihi ngeni kwa kutumia tafsiri ya
Kiingereza”. Hii inaonyesha kuwa alikiangalia zaidi Kiingereza ambayo ni lugha
ya Kiulaya na kutotilia maanani lugha zingine.
(vi). Udhaifu mwingine upo katika fasili yao ya fasihi
linganishi kuwa ni taaluma inayohusika na kulinganisha kazi mbili au zaidi. Ni
ngumu kulinganisha kazi zaidi ya mbili kwa sababu katika ulinganishaji wa kazi
kwa mfano kazi tatu, kutakuwa na sifa ambazo zinafanana kwa kazi mbili na
katika kazi ya tatu sifa hizo hazipo. Kwa hiyo inakuwa ngumu kutoa hitimisho
juu ya kazi hizo kwani zinafanana kwa sifa zipi na zinatofautina katika sifa
zipi.
MAREJELEO
Remak. H.H. (1971) “Comparative
Literature :Its definition and function’’ (Method and Parspective), Edited
by Newton.B.Stalknecht and Horst Frenz, USA October 1973. http://www.ocia.org
Rene H.H. Wellek,
First Edition (1949) Theory of Literature. Published by Suprome Council for Literatures,
Arts and Social Science .Domascus 1972.
Wamitila K.W (2003), Kamusi
ya Fasihi,Istirahi na Nadharia, Nairobi: Kenya.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni