DHANA YA FASIHI LINGANISHI
Ponera (2014) akimnukuu Stallknecht (1961) Fasihi linganishi
ni uwanja wa kitaaluma unaoshughulika na fasihi mbili au zaidi zinazohusisha
vipengere tofauti vya kitamaduni. Anaongeza kusema kuwa fasihi linganishi
hujihusisha na uchunguzi na ulinganishaji wa aina mbalimbali ya sanaa, kwa
mfano, uhusiano wa filamu na muziki au fasihi na uchoraji.
Zepetnek (1996) akinukuliwa na Ponera (2014), Fasihi
linganishi ni taaluma inayojihusisha na uteuzi, na uchambuzi wa vipengere
mbalimbali vya kazi ya fasihi kama vile kanuni, mafundisho, na tamaduni ambavyo
vinapatikana katika kazi za fasihi za jamii mbalimbali.
Wamitila (2003), Fasihi linganishi huhusisha uchunguzi wa
maandishi ya wakati mmoja, aina moja na katika lugha mbalimbali kwa nia ya
kumulika sifa inayohusisha kama athari, vyanzo, sifa zinazofanana tofauti za
kiutamaduni. Anaendelea kusema inawezekana kufanya hivyo pia kwa nia ya
kuangalia matapo mbalimbali, maendeleo au hata nadharia za kiuhakiki, fasihi ya
namna hii iliwekewa misingi na juhudi za wana isimu kuanzia kulinganisha lugha
mbalimbali katika karne ya 19.
Boldor (2003) akimnukuu Compbell (1926) Anaeleza kuwa fasihi
linganishi ni taaluma inayochunguza uhusiano uliopo baina ya faasihi mbili au
zaidi nje ya mipaka ya kitaifa kwa njia ya kulinganisha mfanano na msigano.
Remak (1971), anafasili fasihi linganishi kama uwanja wa
kifasihi unaohusika na uchunguzi na mahusiano ya kifasihi nje ya mipaka ya nchi
moja, pia kati ya fasihi na fani nyinginezo.
Hivyo, fasihi linganishi ni uchunguzi wa maandishi
na masimulizi ya wakati mmoja na katika lugha mbalimbali kwa kuhusisha au
kuangalia matapo mbalimbali, maendeleo au nadhariaa za uhakiki ambapo kufanana,
kutofautiana na hata ubora na udhaifu huzingatiwa.
MKONDO WA KIFARANSA KATIKA KUITAZAMA FASIHI LINGANISHI
Huu ndio mkondo wa kwanza kuibuka na kuanza kushughulikia
masuala yahusianayo na taaluma ya fasihi linganishi. Mkondo huu ulianza huko
Ufaransa mwishoni mwa karne ya 19 katika chuo cha Sarborne, uliendelea kushika
hatamu hadi wakati wa vita vya kwanza vya dunia. Mkondo huu ulikuwa maarufu kwa
jina shule ya Kifaransa (French school)
ambapo wadau wake walianzia katika wazo la kutafuta ithibati za chanzo na
athari za kazi mbalimbali za kimataifa. Wao walijikita katika kuchunguza jinsi
mawazo ya kisanaa pamoja na motifu zake zilivyokuwa zinaenea kutoka sehemu moja
hadi nyingine (Ponera 2014).
WAASISI WA MKONDO WA
KIFARANSA
Waasisi wa mkondo huu ni Jean Marie Carre, Marius Francois
Guyard na Tieghem. Licha ya kuwepo kwa waasisi hawa, pia kuna wanafasihi
waliosaidia kukuza na kuendeleza mkondo huu kama vile, Abel Francois Villmain
ambaye aliandika kitabu kiitwacho “literature compare”. Wengine ni Jacques Derrida,
Piere Bourdien, Lucien Goldman, Auguste Comte, Fredric Mistral na Sullt
Prunghomme. Wadau hao walifanya shughuli zao za chini ya jumuiya yao
iliyojulikana kama “French Comperative Literature Association (FCLA)” (Ponera
2014).
FASILI YA FASIHI LINGANISHI
KWA MKONDO WA KIFARANSA
Wao wanafasili fasihi linganishi kama ni utanzu wa fasihi
ambao hujikita katika kutafuta mahusiano mwafaka kati ya fasihi mbili au zaidi
ambazo zina asili tofauti kijamii na kiuwasilishaji (kilugha).
Jean Marie Carre anafasili fasihi linganishi kama utanzu wa
historia ya kifasihi kwa kuwa hushughulikia ulinganishi wa misukumo ya kijamii
au mataifa.
Kwaupande mwingine, wafuasi wa mkondo huu wanaongeza kuwa
taaluma hii hainabudi kufanyika miongoni mwa jamii mahususi.
Tieghem anaifasili fasihi linganishi kwa kuitenganisha na
fasihi kwa ujumla, yeye anasema kuwa tafiti zote zinazochunguza uhusiano wa
sifa jumuishi baina ya fasihi anuai huitwa fasihi kwa jumla. Lakini fasihi
linganishi kama uchunguzi wa kazi mbili (vitabu viwili, watunzi wawili, makundi
mawili ya vitabu au watunzi).
Guyard kwa upande mmoja anakubaliana na Remaki (remaki
alisema juu ya fasihi linganishi na fasihi kwa ujumla hazitenganishiki) kuwa
fasihi kwa ujumla na fasihi linganishi hazitenganishiki, zote zinaongozwa na
methodolojia ya kiulinganishi. Kwa upande mwingine anakubaliana na hoja ya Tieghem
kuhusu fasihi kwa ujumla na fasihi linganishi kuwa mtazamo wake unatoa mawanda
mapana na angavu zaidi kuhusu fasihi ya jumla kuliko faishi ya kitaifa na
fasihi linganishi.
MISINGI YA FASIHI
LINGANISHI KWA MKONDO WA KIFARANSA
(a) Mipaka ya kijiografia na kilugha au kiisimu
Fasihi linganishi inapaswa kuhusisha fasihi za mataifa au
jamii mbili ambazo zinatofautiana kijiografia pamoja na kutofautiana kiisimu au
kilugha; fasihi ya Kiswahili ilinganishwe na fasihi ya Kirusi, Kitaliano na
Kichina, lakini huwezi kufanya ulinganishi baina ya fasihi moja, mfano mtu
kufanya ulinganishi kati ya riwaya za Shabani dhidi ya riwaya za Ephrais
Kezilahabi.
(b)Uchunguzi uwili.
Fasihi linganishi inahitaji kuhusisha kazi mbili za fasihi,
kazi moja haiwezi kufanyiwa uchunguzi wa kiufasihi linganishi, lazima kuwepo na
vitu viwili vinavyohesabiwa kijiografia na kiisimu. Hivyo ili kufanya
ulinganishi ni lazima kuwepo na kazi mbili zilizotofautiana kiisimu na
kijiografia, mtu anaweza kufanya ulinganishi kati ya riwaya za wamitila dhidi
ya riwaya za Shark Spear.
(c) Fasihi zenye watunzi mahususi
Katika kufanya ulinganifu ni lazima kazi zinazotumika au
zitakazotumika ziwe ni fasihi andishi tu, hivyo kazi za fasihi simulizi ambazo
kimsingi watunzi wake hawafahamiki hazitahusika katika taaluma ya fasihi
linganishi.
(
d)Taathira ziletwazo na
vichocheo nje katika fasihi.
Kwa namna gani fasihi ya taifa moja imeathiri fasihi
nyingine, kwa namna gani utamaduni wa taifa fulani umeathiri fasihi na
utamaduni wa taifa jingine, matini husika za fasihi hazichunguzwi kiundani,
msisitizo upo katika maudhui zaidi kuliko fani.
NYANJA ZA FASIHI LINGANISHI
KWA MKONDO WA KIFARANSA
Wanafasihi wa mkondo wa Kifaransa walifanyia kazi katika
vipengere vya taathira, Upokezi, Mwigo, Uazimaji na ushirika sawia usioepukika
kama nyaja za fasihi linganishi;
USHIRIKA SAWIA USIOEPUKIKA KATI YA NYANJA ZA FASIHI
LINGANISHI
Katika Nyanja hizo ambazo ndizo wanamkondo wa Ufaransa
walizozitalii zaidi walionyesha ni kwa jinsi gani mikondo hiyo hushirikiana katika
kukamilishana.
Ulrich Versstein anatoa rai kuwa kuna taathira, mwigo na
uazimaji, lakini pia kunatofauti baina ya michakato hiyo kama ifuatavyo;
Taathira
Kwa mtazamo wa mkondo huu, taathira ni msambao au kusambaa
kwa wazo, dhamira, taswira au jadi fulani ya kifasihi toka kazi moja ya
kifasihi kwenda katika kazi nyingine ya kifasihi (kwa kujua au kutojua).
Zipo taathira za namna nyingi katika fasihi kama ifuatavyo:
A.
Taathira za kifasihi na zisizo za kifasihi
Hizi huchunguza na kufafanua chimbuko la mahusiano sawia
baina ya fasihi mbili au zaidi. Mfano, ushairi wa Kiswahili na ushairi wa
Kiarabu ni za kifasihi lakini ushairi wa Shabani Robert na utamaduni wa
kiislamu si za kifasihi. (hii imepuuzwa sana na mkondo wa Kifaransa kwa maana
ya kwamba msanii anatumia taathira zisizo za kifasihi kama malighafi katika
kuunda kazi mpya).
B.
Taathira za moja kwa moja au zisizo za moja kwa moja
Taathira isiyo ya moja kwa moja hutokea pale moja ya njia
zifuatazo zitasababisha mwingiliano baina ya kazi za kifasihi, ziara za mtunzi,
mapokeo simulizi ya kijadi, hojaji mbalimbali na shajara za watunzi binafsi.
Pia taathira ya moja kwa moja hutokea pale kunapokuwepo na mtaguso halisi baina
ya wanaoathiriana. Mitagusano halisi huweza kutokea kwa mtunzi mmoja kusoma
kazi ya mtunzi mwingine, mtunzi mmoja kuonana ana kwa ana na mtunzi asilia,au
mtunzi mmoja kuwasiliana na mtunzi mwingine kwa njia yoyote ya kimawasiliano.
C .
Taathira chanya na taathira hasi.
Kitendo cha mtunzi wa kazi ya fasihi toka taifa fulani
kutumia vipengere vya fasihi toka fasihi ya taifa linguine katika kuumba fasihi
bora na fanikivu ya taifa lake ni ishara ya taathira chanya, mtunzi wa kazi ya
kifasihi pia anaweza kuandika kinyume na kazi fulani au kwa kutengua kanuni na
maudhui yaliyoelezwa katika fasihi ngeni itakuwa ni ishara ya taathira hasi
katika fasihi.
UHUSIANO WA TAATHIRA NA
MICHAKATO MINGINE
Mchakato wa kitaathira unahusiana sana na michakato ya
upokezi, mwigo na uazimaji.
(i)
Taathira na upokezi
Hakuna taathira zinazoweza kutokea kati ya mtunzi mmoja na
mwingine pasipo upokezi wa kazi ya kisanaa toka nje ya mipaka ya kitaifa.
Upokezi unaweza kuitwa kuwa ni mchakato mmojawapo kuelekea katika taathira.
Upokezi wa kazi ngeni ya kisanaa katika taifa haina maana wala
hailazimishi kuwa hiyo ni ishara njema ya athari chanya. Mchakato wa kiupokezi
si wa kiholela au bahati mbaya, bali ni mchakato wenye utaratibu mahususi kwa
kuwa unatokea pale tu kazi ngeni inapoleta tija za kiutamaduni na kiitikadi
zinazoafikiana na taifa husika.
(ii)
Taathira na mwigo
Taathira ni zaidi ya mchakato au kitendo cha kuiga ama
kuchukua vipengere fulani vya fasihi ngeni katika fasihi ya taifa mahususi.
(iii). Taathira na uazimaji
Si lazima mchakato wa uazimaji vipengele vya kifasihi toka
eneo moja hadi jingine uonekane kama ni uumbaji upya wa vipengele hivyo, ila
uazimaji unaweza pia kuonekana kama uumbaji wa dhana na maudhui mapya kabisa
lakini yenye kuchimbuka au yenye asili toka katika fasihi ngeni. Muhimu ni
kuwa, vipengele vya taathira ya fasihi ngeni katika taifa fulani hubebwa ndani
ya matini husika. Mhakiki anapaswa kuchunguza au kuchanganua kwa makini matini
nzima na azingatie au atilie maanani mchakato wa taathira katika fasihi husika.
Mchakato huo unaanzia katika tafsiri ya kazi ya fasihi ngeni kupitia michakato
ya uigaji na uazimaji.
Uazimaji hutazamwa kama ufafanuzi wa mwigo katika mawanda
mapana. Uazimaji unaweza kuwa upangiliaji upya wa vipengele bora vya fasihi
ngeni katika namna ambayo haipendezeshi zaidi fasihi ya taifa. Katika uazimaji,
mtu anafananishwa na mtafsiri ambae anafungwa na umbo la matini chanzi au
asilia, lakini katika uigaji, mtunzi hafungwi na umbo la matini asilia.
Michakato yote miwili katika fasihi linganishi inaweza kufikiriwa kwa namna
mbili;
(a). Ubunifu wa kisanaa
Fasihi iliyoathiriwa hupokea au huchukua mbinu mpya toka
katika fasihi ngeni (iliyoathiri).
(b). Wizi wa kitaaluma
Kuazima vipengele vya fasihi toka fasihi ngeni pasipo
kurejelea vyanzo husika, hali hii huitwa wizi wa kitaaluma.
UBORA WA MKONDO WA
KIFARANSA KATIKA FASIHI LINGANISHI
(i). Mawazo yao mengine yalihusu kuithamini lugha kama
nyenzo muhimu katika utendaji wa sanaa yoyote, hivyo mtu anapofanya ulinganifu
wa kazi za kifasihi lazima awe na umilisi wa lugha ya kazi husika.
(ii). Waliamini kwamba kila jamii ina kaida zake za
kimaisha, hivyo nivyema kuzingatia historia au utamaduni wa mtunzi wa kazi
husika unapolinganisha na kazi zingine za kifasihi.
(iii). Waliamini kuwa fasihi linganishi ni lazima ionyeshe
ulinganifu mkubwa wa kijiografia kutoka jamii ya msanii mmoja hadi jamii ya
msanii mwingine.
(iv). Pia waliamini kuwa fasihi linganishi ilenge mambo
yanayotendeka kila siku katika jamii kwa lengo la kuonesha ubora, uzuri, ubaya
na namna ya kuboresha kaida za utamaduni, lugha, siasa na uongozi katika jamii.
(v). Mkondo huu ndio ulitoa nafasi au mwanya kwa mikondo
mingine au mataifa mengine kujikita zaidi katika fasihi simulizi.
MAPUNGUFU YA MKONDO WA
KIFARANSA KATIKA FASIHI LINGANISHI
(i). Mkabala huu umemakinika zaidi na vichocheo vya nje
vinavyoathiri fasihi za mataifa mawili au zaidi, hatimaye umeifanya taaluma ya
fasihi linganishi itawaliwe au iongozwe na mbinu za zamani za kiuchunguzi au za
kihistoria na kichanya.
(ii). Mkabala huu umening’iniza fasihi linganishi katika
mipaka ya kiisimu na kimahali baina ya fasihi, unawafanya wanafasihi waendelee
kuichunguza fasihi katika mlengo wa
kimagharibi.
(iii). Mkabala huu unatenganisha au unashindwa kuweka bayana
mpaka au mipaka baina ya fasihi kwa ujumla na fasihi linganishi.
(iv). Mkondo huu hauruhusu kazi za kifasihi zitokazo katika
taifa moja kufanyiwa uchunguzi linganishi.
(v). Misingi inayoelekezwa na mkabala huu inatenganisha
baina ya vichocheo nje na vichocheo ndani (fani na maudhui) vya kazi ya fasihi.
Hatuhitaji kuchunguza kwa undani matini zenyewe za kifasihi, bali tunapaswa
tuchunguze mambo yatokayo nje ya jamii husika na namna yalivyochochea kuibuka
na kufifia kwa vipengere anuai vya kifasihi.
MAREJELEO
Ponera, S. A. (2014), Utangulizi
wa Nadharia ya Fasihi Linganishi: Dar es salaam. Tanzania.
Remak. H.H. (1971) “Comparative
Literature :Its definition and function’’ (Method and Parspective), Edited
by Newton.B.Stalknecht and Horst Frenz, USA October 1973. http://www.ocia.org
Rene H.H. Wellek,
First Edition (1949) Theory of Literature , Translated into Arabic by Muhy Uddin Subhi,
Published by Suprome Council for Literatures, Arts and Social Science ,Domascus
1972.
Wamitila K.W (2003), Kamusi
ya Fasihi,Istirahi na Nadharia, Nairobi: Kenya.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni