Jumanne, 13 Novemba 2018

FASIHI - Uchambuzi wa maana ya Fasihi kwa mujibu wa K.W Wamitila


MAANA YA FASIHI KWA MUJIBU WA K.W WAMITILA

Wataalamu wengi wa fasihi wametoa maana ya neon fasihi kulingana na mitazamo yao,ubunifu wao, falsafa zao na hata uzoefu wao katika uwanja wa fasihi. Makala hii, imeangazia zaidi katika kuichambua maana ya fasihi iliyotolewa na mwana fasihi Kyallo Wadi Wamitila katika kitabu chake cha Kamusi Ya Fasihi; Istilahi na Nadharia, kilichochapishwa mwaka  2003.

Maana ya Fasihi kwa mujibu wa Wamitila (2003)
“Fasihi ni kazi za kisanaa au zilizotumia lugha kwa usanii na zinazowasilisha suala fulani pamoja kwa njia inayoathiri, kugusa na huacha athari fulani na uonyesha ubunilizi na ubunifu fulani na zinazomhusu binadamu”

Fasihi ni kazi ya Kisanaa na yenye kutumia lugha
Hii ina maana kuwa, fasihi ni sanaa kama zilivyo sanaa zingine kama vile muziki, uchoraji, ususi, ufinyanzi n.k, isipokuwa fasihi inatumia lugha ili kufikisha ujumbe wake, tofauti na matawi mengine ya sanaa.

Fasihi ni kazi inayowasilisha suala fulani pamoja
Fasihi ni lazima iwe na mada, jambo au tukio mahususi ambalo inawasilisha, na jambo hilo ni lazima liwasilishwe kwa pamoja. Hii ina maana kuwa, kama jambo au kisa ni lazima kiwasilishwe chote kwa mtiririko unaofaa na uwe ndani ya kazi moja.

Iwasilishwe kwa njia inayoathiri na kugusa
Lengo la msanii ni kuufikisha ujumbe katika jamii kama jinsi yeye anavyohitaji ufike au zaidi yahata ambavyo yeye anahitaji ufike. Ili lengo hilo lifanikiwe, ni lazima kutumia njia zenye kuweza kumgusa msomaji na kuikonga vyema nafsi na moyo wake kwa kile msanii alichokiwasilisha. Kwa mfano, msanii anahitaji kuwasilisha ujumbe juu ya unyanyasaji unaofanywa na baadhi ya viongozi katika nchi, itambidi msanii atumie sauti za hudhuni zilizojaa manyanyaso na uteswaji uliokithiri

Fasihi huacha athari
Kutokana na uhalisia wa fasihi katika jamii nyingi, basi kazi ya fasihi huweza kusababisha matokeo yoyote kutokea katika jamii. Hii ina maanisha kuwa ujumbe umefika mahali ulipotakiwa kufika na ndiyo maana ukasababisha matokeo kutokea.

Ubunilizi na ubunifu
Ubunilizi na ubunifu ni vipengele muhimu sana katika kazi yoyote ile ya fasihi. Fasihi bila ubunifu ni sawa na makala, kama zilivyo makala zingine. Ni vigumu kujihakikishia usalama kwa msanii wa fasihi pasipo kutumia ubunifu. Tukumbuke kuwa, katika jamii kuna makundi ya aina nyingi, hivyo lazima kazi ya fasihi iibue ukinzani endapo kama unakosoa matabaka yenye nguvu.

Zinazomhusu binadamu
Fasihi ni zao la jamii, hivyo ni vyema kazi za fasihi zimhusu zaidi binadamu kwani ndiye mwenye utashi na akiri yenye uwezo wa kufikiri. Hii haina maana kuwa wahusika wanyama hawahitajiki, lahasha! Kinachozungumziwa hapa ni ujumbe umuhusu binadamu.


Marejeo
Wamitila K.W (2003) Kamusi ya Kiswahili; Istilahi naNadharia.Focus
                   Publication.Nairobi.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

MUINGILIANO KATI YA SEMANTIKI NA PRAGMATIKI---ACADEMICIAN BLOG

UTANGULIZI Maana ya Semantiki Richmond (2012   anafafanua maana ya Semantiki kwamba ni tawi la isimu ya lugha linalohusu viyambo ...