Jumatano, 28 Novemba 2018

MJASIRIAMALI--TOP 10 ZA KUKUPA MTAJI KWA HARAKA


#1: Taaluma uliyonayo (elimu)

Unaweza kupata mtaji kwa kuitumia vyema elimu yako! Kuna mambo mawili ya kufanya ili upate mtaji katika njia hii. Mosi, ni kujiajiri mwenyewe kupitia taaluma uliyonayo.
Mfano.
1.       kama wewe ni muhandisi wa umeme, basi unaweza ukaanzisha huduma ya kuweka umeme majumbani (domestic electirical installation). Kupitia hii huduma, unaweza kupata mtaji na kisha ukafungua duka la vifaa vya umeme. Ni watu wengi waliofanikiwa kupata mitaji mikubwa kwa kupitia njia hii! Nina mfano wa technician mmoja wa kiwanda cha saruji kilichopo Songwe- Tanzania (Zephania Lulyeho), yeye alianza kufanya hivyo kama anajaribu, lakini sasa hivi anamiliki kampuni yake ya JAZA yenye kujishughulisha na masuala ya kufanya electrical installation.
2.       kama wewe ni daktari, basi unaweza kuanzisha kituo kidogo cha afya! Hata kama kiwe na uwezo wa kutoa huduma ya kwanza, au kutoa vipimo hata viwili (mf, malaria na taifodi) kinatosha kuanzia. Baada ya kupata mtaji mzuri, basi utaweza kufungua duka la madawa! Kwani utakuwa tayari una cheti cha afya, lakini pia utakuwa na kibari cha kukuruhusu kuuza madawa na vyakula, mfano cheti cha TFDA kwa upande wa Tanzania.
3.       kama wewe ni mwalimu, basi unaweza ukaanzisha kituo cha masomo kwa muda wa ziada (tution). Kituo hiki utakipatia majukumu kadha wa kadha kama vile, kozi fupi ya lugha ya Kiingereza, kuwanoa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na Kuwanoa wale wanaohitaji kurudia kufanya mitihani ya kidato cha 4 & 6. Haya majukumu ni vigumu kufanywa na mtu mmoja kwa ufanisi, hivyo unashauriwa kuungana na watu wenye nia na wenye vigezo vya kufanya kazi hiyo, hata kama iwe nikwakugawana faida.
Lakini, pili (2) ni kuajiriwa katika taasisi, serikali ama mtu binafsi

#2: Kuomba mtaji kwa wanafamilia, ndugu na jamaa

 Hapa pia kuna mambo ya kuzingatia ili upate mjati kwa ndugu au jamaako wa karibu
v  Onyesha uwajibikaji
v  Msaidie kazi kwa uaminifu wote
v  Tambua nini anapendelea huyo ndugu yako  
v  Mpe mawazo na mbinu za kuiendeleza biashara yake
v  Utakapofikia wakati wa kumwomba mtaji, omba mtaji kidogo
v  Baada ya kupewa mtaji, hakikisha unamshirikisha katika biashara yako. Hii ni pamoja na kumpatia taarifa juu ya maendeleo ya biashara yako.

#3: Fani/ kipaji

Unaweza kupata mtaji kupitia kipaji chako! Lakini pia unaweza kukifanya kipaji chako kama ndiyo ajira yako. Ili kukifanya kipaji kuwa ajira, unashauriwa pia kupata mawazo mapya kutoka kwa watu, wateja, au washabiki wako, lakini pia soma vitabu mbali mbali vinavyohusiana na kipaji chako. Mawazo haya ndiyo yatakayokufanya uwe mbunifu katika fani yako. Unapofanya kazi kupitia kipaji chako, ni vyema pia ukazingatia uhusiano wa kazi zako na soko la kimataifa. Katika makala zijazo, tutajadili zaidi juu ya jinsi ya kutafuta masoko ya kimataifa kwa lazima. Mfano, msusi, mfinyanzi, mchoraji, mchongaji, mwana muziki, mwandishi nk, hawa wote wanawezaje kupata soko la kimataifa kwa lazima. Maana, inatakiwa umlazimishe mtu kuwa mteja wako pasipo yeye kujua kama unamlazimisha kuwa mteja wa bidhaa yako.

#4: Uzoefu katika kufanya kitu fulani

Katika upande wa masuala ya ajira imekwisha zoeleka kwamba, ili upate ajira basi unatakiwa uwe na uzoefu wa miaka kadhaa kazini katika kitengo unachoomba kazi. Ukweli ni kwamba katika mfumo wa uchumi na biashara kwa sasa, mwajiri anaajiri mtu ambaye anaweza kumrahisishia kazi bila kufundishwa pindi anapokuwa akitumikia nafasi yake ya kazi ili kuepusha hasara na gharama ambazo hazikuwa za lazima. Lakini pia, hauwezi kupata uzoefu bila kuanza. Hii nina maana kwamba, ili upate uzoefu basi fanya kazi hata kwa mfumo wa kujitolea, kwani kupitia kujitolea utaweza kujuana na watu wengi zaidi na zaidi, na hicho ndicho mshahara wako.

#5: Ujuzi

Ujuzi nao ni moja ya mambo muhimu sana katika kukurahisishia kupata mtaji. Hapa zaidi kinachotiliwa maanani ni ufundi ambao mtu anaupata hata pasipokuwa na elimu kubwa. Kupitia ujuzi, unaweza kuwa fundi ujenzi wa kisasa, fundi wa vifaa vya kielekitroniki kama vile, redio,TV,kompyuta,pasi za umeme n.k. watu wengi sana wana ujuzi mbalimbali, lakini hawana nidhamu ya pesa. Kutokuwa na nidhamu ya pesa, kunawafanya wawe na maisha yale yale kila mwaka, na hatimaye kuuona ujuzi wao kama hauwasaidii kabisa katika maisha yao! Jamani TUBADILIKE KATIKA JINSI YA KUFIKIRI MAMBO

#6: Fanya Kitu unachokipenda

Kufanya kitu unachokipenda ni njia mojawapo muhimu ya kukuongezea mtaji. Kuna watu wana mitaji midogo na wameshindwa kuiendeleza mitaji hiyo kutokana na kufanya kitu/biashara wasioipenda. Ni ukweli kuwa, kuna baadhi ya watu hufanya mambo, kazi au biashara kwa kufuata mihemko ya wazazi, ndugu au rafiki zao, lakini ndani ya moyo mioyo yao hawaridhiki kabisa. Hali hii itakufanya upunguze ukaribu na kile unachokifanya, lakini pia unaweza kukosa ubunifu wa kazi/ biashara hiyo kutokana na kutoipenda.

#7: Omba mkopo

Kama una nia kweli ya kufanya biashara, na una vigezo vya kuzifanya taasisi za kifedha kukuamini, bai omba mkopo.
ANGALIZO: 1
Usiombe mkopo wa kibiashara, endapo kama haujaanza biashara, maana fedha ya mkopo siyo fedha ya kuanzisha biashara, bali ni fedha ya kuendeleza biashara. Nimeeleza mambo mengi sana katika kitabu change kinachohusu masuala ya mikopo, na siku siyo nyingi nitakichapisha ili nawe msomaji wangu ujifunze mengi juu ya masuala ya mikopo kutokana na mengi niliyojifunza kuhusu mikopo.

ANGALIZO: 2
Usichukue mkopo endapo kama haujafanya utafiti wa kutosha juu ya biashara unayoifanya/unayotaka kuifanya.

#8: Uuzaji wa rasilimali

Hii nayo ni njia ya kupata mtaji lakini sikushauri sana kuitumia kwani, siyo rahisi kuirudisha rasilimali ambayo umekwishaiuza. Kama mtu unayeanza kupambana ili upate msingi mzuri wa maisha, si vyema kuwa na tabia ya kuuza vitu. Hii ni kutokana na ukweli kuwa, bei utakayouzia kwa kiasi kikubwa siyo bei rafiki. Lakini kama ukikwama sana na ukaona njia zingine huwezi kuzitumia basi unaweza ukauza, lakini uwe na uhakika wa kuirusha rasilimali hiyo unayoiuza.

#9: Kushirikiana na watumishi wa serikali

Kuna baadhi ya watumishi wa serikali hawana muda wa kuzalisha mishahara yao. Lakini wapo wengine ambao hata hawana elimu ya fedha. Kutokana na pengo hili, kama mjasiliamali usiye na mtaji, unatakiwa kupanga biashara na mwelekeo wa hiyo biashara, na kisha ukamshirikisha mtumishi ambaye anaonekana kutokuwa na uwekezaji wowote wa fedha yake.
ANGALIZO
Mjasiriamali unatakiwa kuwa na tarifa za uhakika juu ya biashara unayoipendekeza, na hizi taarifa unaweza kuzipata kupitia kufanya utafiti wa kutosha juu ya biashara hiyo. Mfano, je ni biashara ya msimu?, faida yake, hasara zake zinasababishwaje? Jinsi ya kuzuia hasara, wateja wa biashara hiyo ni watu gani? N.k. kwa kufanya hivyo, utaweza kufanya biashara ambayo itakunufaisha wewe pamoja na Yule aliyewekeza fedha yake katika biashara hiyo.

#10: Ufugaji

Kama una mtaji wa eneo, basi fanya ufugaji wa mifugo ili upate mtaji unaouhitaji ndani ya kipindi kifupi. Kuna mifugo wengi ambao unaweza ukawafuga, mfano, kuku wa kienyeji, bata wa kawaida, bata maji, bata mzinga, sungura, kanga, kwale, nguruwe n.k. hawa wote wana uwezo wa kukupatia mtaji kwa muda mfupi. Cha muhimu ni kufugakibiashara, na kutafuta masoko yenye tija.
Katika biashara, mambo ya muhimu unayotakiwa kuwanayo ni UKWELI na UAMINIFU! Utapata wateja waminifu na utapata mtaji hata bila kuomwomba mtu, ila yeye atakuletea fedha yake uifanyie uzalishaji

Nakushukuru kwa kufuatilia makala zangu katika blog yangu na katika kurasa zangu za mitandao ya kijamii. Usikose kufuatilia makala zangu zingine, ni rahisi sana, ingia kwenye blog yangu kisha bofya kitufe  follow by e-mail. Mpaka hapo utakuwa umefanikiwa kupata makala zangu mpya.

Jumanne, 27 Novemba 2018

UJASIRIAMALI--JINSI YA KUPATA MTAJI BILA KUKOPA


JINSI YA KUPATA MTAJI KWAAJILI YA KUANZISHA BIASHARA BILA KUKOPA (MKOPO)
Kabla ya kujifunza kitu chochote katika makala hii, ni vyema tukajuzana kuwa, biashara haihitaji haraka kama jinsi tunavyoichukulia biashara. Biashara inahitaji utaratibu wa hatua kwa hatua, huku ukifanya tathmini kwa kila hatua (yaani unaangalia mafanikio, changamoto,  mapungufu na namna ya kutatua vizuizi vinavyojitokeza katika biashara).
Mjasiriamali mdogo anashauriwa kuanza na mtaji mdogo na kisha kuukuza mtaji huo kidogo kidogo. Ni rahisi kufikia malengo yako kibiashara endapo kama utaona kila fedha inafaa kuwa mtaji kwa kuanza biashara. Kwa mfano, umepanga kuwa, baada ya miezi mitatu (3) inatakiwa upate shilingi 1,000,000/- (Milioni moja), ili kuanzisha biashara ya kusafirisha mazao kutoka vijijini na kuyapeleka mjini, huku ukiwa na shilingi 50,000/- (elfu hamsini) mfukoni  mwako. Lakini cha kushangaza, baada ya miezi mitatu ya malengo, unajikuta una shilingi 100,000/- (Laki moja tu) ama chini ya hicho kiasi. Kwa muonekano huo, utakuwa umefeli kabisa kupata shilingi 1,000,000/- kwaajili ya kuanzisha biashara ya kusafirisha mazao mjini.
# Kosa limetokea wapi?
Kimsingi fedha ya biashara haitakiwi kukaa bila kuzungushwa na kuleta faida. Kumbe basi, ilitakiwa ile ile shilingi 50,000/- (elfu hamsini) uitazame kama mtaji unaofaa kuanzisha biashara ndogo yenye uwezo wa kukupatia hata faida ya shilingi 15,000/- (elfu kumi na tano) kwa siku. Kuna biashara nyingi za kuweza kukupatia hicho kiasi cha pesa kwa siku endapo kama utakuwa tayari kufanya kazi kwa bidii na kujituma. Kwa mfano, unaweza ukaenda soko kuu lolote lililo karibu, kisha ukanunua matunda ya shilingi 50,000/- kwa bei ya jumla na kisha ukayauza kwa  wanaojua nini maana ya matunda, ungeweza kupata faida ya shilingi 20,000/- kwa siku Hii ingekujengea msingi na mwanzo mzuri katika safari yako ya kuitafuta shilingi 1,000,000/- kama mtaji wa kuanzisha biashara ya kusafirisha mazao kutoka vijijini na kuyapeleka mjini. Hii inawezekanaje? Tuangalie hesabu ndogo hapa chini.
Kwa masoko makubwa yaliyomengi nchini Tanzania, bei za jumla za matunda ni kama ifuatavyo;-
*      Chungwa  1= shilingi 100/=, na unaweza kuuza kwa bei ya machungwa 6 = shilingi 1,000/=
*      Maembe  3 (ya ukubwa wa wastani ya kati) = shilingi 500/=, na unaweza kuuza kwa bei ya shilingi 1,000/= (elfu moja, kwa fungu la maembe 3)
*      Tikiti maji 1 (la saizi ya kati) 2,000/= hadi 3,000/=, na ukaweza kuuza kwa bei ya shilingi 4,000/= hadi 5000/= (Isipokuwa kwa mikoa ya Dae-es-Salaam, Arusha, na Pwani) kwa upande wa Tanzania,
*      Parachichi 3 (za ukubwa wa wastani ya kati) = shilingi 500/=, na unaweza kuuza kwa bei ya shilingi 500/= kwa kila parachichi 1, au kwa bei ya shilingi 1,000/= kwa fungu la parachichi 3.
Je, hii siyo faida? Na pia, ngoja nikupe siri hii msomaji wangu! Hakuna biashara iliyonzuri kama biashara inayokupatia faida inayolingana na mtaji, au faida inayozidi mtaji uliowekeza, haijalishi ni kiasi gani cha mtaji ulichowekeza. Katika biashara, unapoongeza wateja wapya, ndivyo unavyoongeza faida zaidi na zaidi.
Kwa mchanganuo huu, nategemea kutosikia neno “sina mtaji” kwa msomaji wangu aliyesoma makala hii, kwani naamini kabisa kuwa, hakuna mtu ambaye anaweza kukosa shilingi 500/= ya kuanzisha biashara ya kuuza matunda kwa watu wanaojua umuhimu wa matunda.
Mtu anawezakuwa na uwezo wa kukusanya faida ya shilingi 50,000/= (elfu hamsini) kama faida ya siku moja, lakini asiwe na maendeleo yoyote. Donald  J.Trump, na Robert  T. Kiyosaki, katika kitabu chao kinachojulikana kama Why We Want You To Be Rich” katika masuala ya maendeleo kibiashara, walisema “Tatizo siyo kwamba tunaingiza shilingi ngapi, bali tatizon ni, tunatunza shilingi ngapi? Lakini pia wote kwa pamoja wanakubaliana kuwa, katika biashara, kwa waliowengi, “Tatizo siyo mtaji! Ila tatizo ni kukosa elimu ya biashara na ujasiriamali” nukuu za waandishi hawa zinadhihirisha ukweli kabisa kuwa, hata shilingi 1,000/= (elfu moja) ni mtaji tosha wa kuanziasha baadhi ya biashara, ila shida kubwa ni kuifanya hiyo shilingi 1,000/= izae na kuleta mtaji mkubwa zaidi.

# ANGALIZO KWA MJASILIAMALI MDOGO (MUUZAJI WA MATUNDA)
Ø  Kama una mtaji mdogo, chonde chonde usifanye biashara ya kusafiri umbali mrefu, bali fanya biashara ya kusafiri kwa umbali usiozidi lisaa limoja. Hii itakurahisishia kuwa na uhakika wa kurudia bidhaa muda wowote utakapomaliza bidhaa, na hivyo kufanya mzunguko wako kwenda haraka,  wenye tija na wenye kukupatia faida zaidi.
Ø  Usikopeshe zaidi ya nusu ya mtaji wako, maana kwa kufanya hivyo, unaweza ukajikuta unakosa fedha ya kwenda kuchukulia mzigo, wakati ukiwa umeshauza mzigo wote (ila kwa mkopo).
Ø  Mkopeshe mteja ambaye una uhakika wa kulipwa ndani ya masaa kadhaa, na siyo siku kadhaa.
Ø  Uwe mwaminifu na mkweli katika biashara zako
Ø  Itetee vyema biashara yako
Ø  Ipende biashara yako, kwa kuiona kama ndiyo kazi yako uliyoajiriwa.
Ø  Uwe na lugha nzuri kwa wateja wako! hata kama hutaki kumkopesha, si vyema ukamwambia kuwa “sikopeshi” badala yake mwambie “kwa kweli leo sina hela ya kwenda kuchukulia mzigo, mzigo huu ndio ninaoutegemea kuongezea mtaji wa leo” mteja huwa ni mwelewa sana endapo kama utatumia lugha ya kumwelewesha kwa utaratibu na bila kuharibu furaha yake aliyonayo siku hiyo.
Ø  Kuwa na bei rafiki na isiyomuumiza mteja (yaani unakuwa na watja wa kila aina, wapo wale wenye uwezo mzuri, pia wapo ambao uwezo wao ni mdogo, ila kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao,inawabidi wapate bidhaa zao ili maisha yaende) kwa mfano, kwa mjasiriamali anayeuza matunda, atakutana na wateja kama vile wagonjwa, wajawazito na wamama waliojifungua siku si nyingi. Hawa wote wanahitaji huduma ya matunda, hivyo ni vyema kwa muuzaji kujua saikolojia na uwezo wa wateja wake.

Nakushukuru kwa kufuatilia makala zangu katika blog yangu na katika kurasa zangu za mitandao ya kijamii. Usikose kufuatilia makala zangu zingine, ni rahisi sana, ingia kwenye blog yangu kisha bofya kitufe  follow  by e-mail. Mpaka hapo utakuwa umefanikiwa kupata makala zangu mpya.

REJEA
Trump, D.J & Kiyosaki, R.T (2006) Why We Want You To Be Reach. Rich Press
                        Publishers.New York.

Jumanne, 13 Novemba 2018

FASIHI - Uchambuzi wa maana ya Fasihi kwa mujibu wa K.W Wamitila


MAANA YA FASIHI KWA MUJIBU WA K.W WAMITILA

Wataalamu wengi wa fasihi wametoa maana ya neon fasihi kulingana na mitazamo yao,ubunifu wao, falsafa zao na hata uzoefu wao katika uwanja wa fasihi. Makala hii, imeangazia zaidi katika kuichambua maana ya fasihi iliyotolewa na mwana fasihi Kyallo Wadi Wamitila katika kitabu chake cha Kamusi Ya Fasihi; Istilahi na Nadharia, kilichochapishwa mwaka  2003.

Maana ya Fasihi kwa mujibu wa Wamitila (2003)
“Fasihi ni kazi za kisanaa au zilizotumia lugha kwa usanii na zinazowasilisha suala fulani pamoja kwa njia inayoathiri, kugusa na huacha athari fulani na uonyesha ubunilizi na ubunifu fulani na zinazomhusu binadamu”

Fasihi ni kazi ya Kisanaa na yenye kutumia lugha
Hii ina maana kuwa, fasihi ni sanaa kama zilivyo sanaa zingine kama vile muziki, uchoraji, ususi, ufinyanzi n.k, isipokuwa fasihi inatumia lugha ili kufikisha ujumbe wake, tofauti na matawi mengine ya sanaa.

Fasihi ni kazi inayowasilisha suala fulani pamoja
Fasihi ni lazima iwe na mada, jambo au tukio mahususi ambalo inawasilisha, na jambo hilo ni lazima liwasilishwe kwa pamoja. Hii ina maana kuwa, kama jambo au kisa ni lazima kiwasilishwe chote kwa mtiririko unaofaa na uwe ndani ya kazi moja.

Iwasilishwe kwa njia inayoathiri na kugusa
Lengo la msanii ni kuufikisha ujumbe katika jamii kama jinsi yeye anavyohitaji ufike au zaidi yahata ambavyo yeye anahitaji ufike. Ili lengo hilo lifanikiwe, ni lazima kutumia njia zenye kuweza kumgusa msomaji na kuikonga vyema nafsi na moyo wake kwa kile msanii alichokiwasilisha. Kwa mfano, msanii anahitaji kuwasilisha ujumbe juu ya unyanyasaji unaofanywa na baadhi ya viongozi katika nchi, itambidi msanii atumie sauti za hudhuni zilizojaa manyanyaso na uteswaji uliokithiri

Fasihi huacha athari
Kutokana na uhalisia wa fasihi katika jamii nyingi, basi kazi ya fasihi huweza kusababisha matokeo yoyote kutokea katika jamii. Hii ina maanisha kuwa ujumbe umefika mahali ulipotakiwa kufika na ndiyo maana ukasababisha matokeo kutokea.

Ubunilizi na ubunifu
Ubunilizi na ubunifu ni vipengele muhimu sana katika kazi yoyote ile ya fasihi. Fasihi bila ubunifu ni sawa na makala, kama zilivyo makala zingine. Ni vigumu kujihakikishia usalama kwa msanii wa fasihi pasipo kutumia ubunifu. Tukumbuke kuwa, katika jamii kuna makundi ya aina nyingi, hivyo lazima kazi ya fasihi iibue ukinzani endapo kama unakosoa matabaka yenye nguvu.

Zinazomhusu binadamu
Fasihi ni zao la jamii, hivyo ni vyema kazi za fasihi zimhusu zaidi binadamu kwani ndiye mwenye utashi na akiri yenye uwezo wa kufikiri. Hii haina maana kuwa wahusika wanyama hawahitajiki, lahasha! Kinachozungumziwa hapa ni ujumbe umuhusu binadamu.


Marejeo
Wamitila K.W (2003) Kamusi ya Kiswahili; Istilahi naNadharia.Focus
                   Publication.Nairobi.



MUINGILIANO KATI YA SEMANTIKI NA PRAGMATIKI---ACADEMICIAN BLOG

UTANGULIZI Maana ya Semantiki Richmond (2012   anafafanua maana ya Semantiki kwamba ni tawi la isimu ya lugha linalohusu viyambo ...