Jumatatu, 29 Aprili 2019

MUINGILIANO KATI YA SEMANTIKI NA PRAGMATIKI---ACADEMICIAN BLOG



UTANGULIZI

Maana ya Semantiki
Richmond (2012  anafafanua maana ya Semantiki kwamba ni tawi la isimu ya lugha linalohusu viyambo vya Lugha.Anaendelea kusema kuwa semantiki ni utanzu wa isimu unaojishuighurisha na maana ya maneno au viyambo vya maneno katika Lugha .  Swali kuu katika wanasemantiki ni  kuhusu nini maana ya maana.Hata hivyo wanasemantiki hujikita katika kuchunguza  maana katika viwango mbalimbali kama vile: ngazi ya sayansi (fonimu),  Neno, Virai, Vishazi na hata sentesi. Anamalizia kwa kusema kuwa tawi hili  la isimu limekuwa ni muhimu sana  hasa kutokana na umuhimu wa mazungumzo kwani ili mazungumzo yaelewekena ujumbe ufahamike panaitajika Maana.
King’ei (2010), Semantiki, ni taaluma ya isimu inayofafanua maana katika lugha.
TUKI (2004), Semantiki, ni tawi la isimu ambalo hujishughulisha na uchambuzi wa lugha katika kiwango cha maana.
Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa Semantiki ni taaluma inayohusika na uchunguzi wa maana katika lugha itumiwayo na mwanadamu.

Maana ya Pragmatiki
Masamba (2004). Pragmatiki (Pragmatics), ni taaluma ya isimu inayojishughulisha na uchunguzi na uchambuzi wa lugha katika mawasiliano. Lengo kuu la taaluma hii ni kuchunguza namna lugha inavyotumiwa na wasemaji wake katika mazingira halisi, kama kwa nini msemaji ameamua kusema hivi badala ya kusema vinginevyo, anakabiliwa na masharti gani ya maamuzi?.
Leech (1981), anasema semantiki inaangalia  maana ya matamshi, maumbo na Miundo katika lugha. Anaendelea kusema  Maana ni sehemu ya umilisi na ufahamu wa lugha, kujifunza Lugha ni kukubaliana na maana za vipengele vyote vilivyopo katika lugha.
Richmond (2012), anasema kwamba ni tawi la Lugha linalojihusisha na matumizi ya lugha kwa kuzingatia Muktadha wa wazungumzaji husika. Hivyo Thomason anadai kuwa pragmantiki inahusu zaidi mambo mawili: Matumizi na Muktadha.
Geoffery (2012), anasema kuwa, dhana ya pragmantiki ilivumbuliwa katika miaka ya 1930 na mwanafalfasa C.W. Morris na imeanza kujulikana kama Tawi tegmezi la isimu lugha miaka ya 1970 ambapo kabla ya hapo pragmantiki ilihusishwa kama tawi la kifalsafa, na kufafanuliwa kwa kuzingatia misingi mikuu miwili : Matumizi na Muktadha.
Kwa upande wake Yule (1996) anafafanua dhana ya pragmantiki kwa kusema kuwa ni taaluma inayohusu mahusiano yaliyopo kati ya Maana ya lugha na watumiaji wa mambo hayo.
Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa Pragmatiki ni taalumainayohusiana na matumizi  halisi ya lugha katika muktadha tofauti  na uelewa wake kama vile malengo ya mzungumzaji na jinsi msikilizaji anavyopokea malengo hayo,Mfano, matumizi ya lugha katika muktadha wa hotelini ambapo mtu anweza kusema nipe chai tatu na akaeleweka

UHUSIANO KATI YA SEMANTIKI NA PRAGMATIKI

A. Kufanana kati ya Semantiki na Pragmatiki

1. Semantiki na Pragmatiki vyote kwa pamoja vinalenga kutoa ufafanuzi kuhusu mchakato wa lugha na matumizi yake kulingana na muktadha wa wazungumzaji au utumikaji wake kama sehemu ya mfumo wa mazungumzo sambamba, kufasili na kufafanua mfumo tungamanifu wa mazungumzo katika lugha, na hili litafanikiwa tu kwa kuzingatia maarifa ya lugha sambamba na ulimwengu halisi wa mazungumzo.

2. Maana ya kisemantiki inaweza kuzalisha maana ya kipragmatiki, hii ina maana ya kwamba  maana inayopatikana katika pragmatiki hutokana na semantiki. Mfano, maana ya kipragmatiki ya neno mtoto kumaanisha mpenzi inatokana na maana ya kisemantiki ambayo ni kiumbe kichanga amabcho kinahitaji matuzo na uangalifu mkubwa katika malezi.

3. Semantiki na Pragmatiki zote kwa pamoja zinahusiana, kwa maana kwamba zinajihusisha na maana ya maana katika lugha. Wala haitokuwa sahihi kudhani kwamba kufahamu tu maana ya viambajengo katika tungo, iwe neno, kirai, kishazi, au hata sentensi kuwa ndio kufahamu kwa kile kilichokusudiwa bila kujali muktadha ambao neno hilo limetumika.Mfano, maana za maneno zinazopatikana katika muktadha mbalimbali kama vile sokoni, shuleni na muktadha mwingine.

4. Kuna baadhi ya dhana za kisemantiki hutegemea msaada wa maana za kipragmatiki ili ziweze kufikisha ujumbe kwa baadhi ya hadhira pasipo kuharibu mazungumzo au kumkwaza msikilizaji. Mfano, mtu anaweza kumwambia mwingine kwenye umati wa watu kuwa funga mlango wako akiwa na maana ya afunge zipu ya sehemu ya siri ili mtu huyo asijisikie vibaya au aibu.

5. Vilevile matawi haya yotekwa pamoja hushughulikia maana kaika lugha. Pragmatiki inashughulikia maana isiyo ya msingi bali maana inayotokana na muktadha, husika.kwa mfanonenomtoto katika muktadha wa kimapenzi ni msichana, wakati semantiki inashughulika na maana ya msingi ambayo inatoa fasiri kulingana na kitu kinachoonekana.kwa mfanonenomtoto litafasiliwa kama ni kiumbe kinacho zaliwa na binadamu ambacho kina umri chini ya miaka kumi na nane.

6. Matawi yote mawili hutumia dhana ya simiotiki ambapo hujaribu kuchunguza uhusiano uliopo kati ya umbo na maana inayopatikana katika umbo hilo. Mfano, alama mbalimbali na matendo halisi ambapo kuna kuwa na uhusiano kati ya maumbo hayo na maana zake.

7. Semantiki na pragimatiki zote zinafanya kazi katika lugha yoyote ile siyo Kiswahili peke yake yaani hazifungwi na mipaka ya lugha yoyote .Mfano; semantiki na pragimatiki zinavyofanya za kuchunguza maana za maneno katika lugha mabalimbali kama vile lugha za kibantu na lugha zingine.

B. Kutofautiana kati ya Semantiki na Pragmatiki

1.Kwa mujibu wa Louise McNally(1993), katika makala yake ya Semantiki na Pragmatiki anasema kuwa, Katika pragmatiki maana hutolewa huku ikihusishwa au kutegemeana na mzungumzaji wa lugha, hii inamaana kuwa katika pragmatiki, maana ya neno au tungo inategemea nini mzungumzaji anakusudia kusema. Mfano, mtu anaweza kusema leo niko ovyo akiwa na maana ya kwamba hana hela WAKATI  katika semantiki, maana hutolewa ikiwa safi na hutolewa kama jinsi inavyopaswa kuwa kutoka katika lugha husika, na maana hiyo ndiyo huchukuliwa kama ndiyo njia ya mawasiliano.Mfano, mtu ana kuwa wazi tu kusema kuwa leo sina hela.

2. Neno katika semantiki ndilo hubeba maana ya msingi na hulenga maana halisi ya neno kama jinsi ambavyo wazungumzaji wa lugha hiyo walivyolizoea toka enzi na enzi. Maana hii ya msingi huwa haibadiliki katika jamii zote zinazotumia neno hilo. Mfano, neno “baba” huwa na maana moja tu ya msingi ambayo ni mzazi wa kiumeWAKATI katika pragmatiki, hali hiyo ni tofauti, ambapo neno hutazamwa katika mtazamo wa kidhima huku likihusishwa na muktadha ambapo neno hilo limetumika.Mfano, neno “mtoto” hubadilika kulinga na muktadha ambapo kwa muktadha mwingine hutumika kama mpenzi Hii ni kwa mujibu wa Carston (1998) na Louise McNally.

3. Katika semantiki, maana hutegemea sheria sinazohusishwa na muundo wa sentensi (sintaksia ya lugha) Hivyo muundo ndio unaoamua na kutoa matokeo ya maana inayokusudiwa msikilizaji aipate. Mfano, unga unaliwa na kuku. Hivyo endapo kama maneno hayo hayo yakiwekwa katika mpangilio tofauti, pia hata maana yake hubadilika LAKINI katika pragmatiki, maana hufinyangwa kutoka katika mazingira halisi ambayo neno husika limetumiwa na haifungwi na sheria za kimuundo. Mfano, mtu anaweza kusema unga unakula kuku kwa sababu hakuna sharia inayomfunga.(Carston, 1998)

4. Carston (1998) na Louise McNally, kwa wakati tofauti wanasema kuwa, tunapotumia sentensi yenye maana tofauti na maana halisi basi aina hiyo ya maana tutaiita kuwa ni maana ya mzungumzaji au maana kutokana na muktadha au maana ya matamshi au pragmatiki. Hivyo kwa ujumla maana hiyo itakuwa ni maana ya mzungumzaji na siyo maana ya jamii nzima.Mfano, mtu anasema leo nimekauka wakati huo akiwa na maana ya kwamba leo sijakunywa pombe ya aina yeyote ile hvyo hiyo itakuwa maana yake na sio ya jamii nzima WAKATI katika semantiki maana inayopatikana katika sentensi, huwa ni maana halisi ambayo kila sehemu huitambua na jamii za aina mbili au zaidi huweza kuwasiliana na kuelewana. Mfano, maana ya neno baba hutambulika kama ni mzazi wa kiume kwa jamii zote.kwa kutumia maana hiyo, hivyo mzungumzaji hujibiwa kama jinsi inavyopaswa kujibiwa kulingana na jinsi neno hilo linavyosimama katika isimu ya lugha hiyo.

5. Matawi haya mawili ya lugha, pia hutofautiana katika wigo wake (scope) semantiki wigo wake ni mfinyu sana kwa sababu inajikita zaidi na kuchunguza maana katika nakala tu, na kuchambua maana ya maneno na jinsi gani maneno hayo yanaungana na kuunda sentensi iliyo na maana.Mfano, semantiki hujikita kuchunguza miundo sahihi ya sentensi kama vile baba analima shamaba au kuku anakula unga, ni miundo ya sentensi ambayo inaleta maana kamili WAKATI  pragmatiki ina uwanja mpana sana kwani inajishughulisha na maeneo mbalimbali zaidi hata ya kuchunguza nakala.Mfano, pragmatiki huchuichunguza namana lugha inavyotumika katika maeneo mbalimbali,mfano katika eno la sokoni mtu anaweza kusema mimi utumbo na akaeleweka. (Alghamdi, 2013)

6. Katika semantiki, muktadha hutegemea zaidi sheria na taratibu za lugha. Hii ina maana kuwa, lugha ndiyo huamua mzungumzaji atumie muktadha upi pindi anapozungumza na hii huambatana na jinsi sheria za lugha zinavyohitaji WAKATI katika pragmatiki, maana ya mzungumzaji hutegemea muktadha husika. Hii ina maana kuwa, muktadha ndio hutawala lugha na kuamua ni tungo ipi itumike katika muktadha fulani, hata kama inapingana na sheria za lugha hiyo (Alghamdi, 2013)

7. Maana ya kipragmatiki kwa kiasi kikubwa huathiriwa na nia au kusudio au saikolojia ya mzungumzaji na siyo kama jinsi ambavyo sentensi inavyomaanisha.Mfano, mtu anaweza kutumia neno ambapo akawa na lengo la kuficha uma isijue nini kinaendelea kwani anaweza kusema umekiona wapi kitabu changu leo wakati huo akiwa na maana ya mpenzi wake WAKATI katika semantiki, kusudio na nia ya mzungumzaji ni sharti ikubaliane na kanuni za lugha husika, ikiwa ni pamoja na kufuata taratibu za muundo wa sentensi yaani mpangilio wa viambajengo katika sentensi.Mfano, mtu ana kuwa huru kuongea kile ambacho anakimaanisha yaani kama ni kitabu basi anakuwa anamaanisha kitabu kweli na sio vinginevyo  (Carston, 1998)

8. Recanati (2002), Jeffrey na Stanley (2003) wanasema kuwa, maana ya kisemantiki haibadiliki badiliki kuendana na wakati (yaani wakati mwingine neno hutumiwa kwa kurejelea maana iliyopita) hii ina maana kuwa semantiki inaweza kutupatia maana ya tendo lililofanyika miaka mingi iliyopita.Mfano, neno hayati hurejea mtu ambaye tayari amekwishafariki na hata kuzikwa pia WAKATI katika pragmatiki, maana hubadilika badilika kuendana na wakati uliopo, na hivyo kujikuta kuwa na utajiri wa maneno au tungo mbalimbali zenye kuelezea tukio linaloendelea kwa wakati uliopo. Kwa mfano, mtu anapokumbushwa kifo cha ndugu yake aliyefariki mwaka mmoja uliopita, na kisha akaanza kutoa machozi. Hii inaonyesha aina mbili za maana kisemantiki na kipragmatiki:
(a)     Maana inayopatikana kutoka katika taarifa kuhusu kifo, hiyo ni maana ya kisemantiki.
(b)    Maana inayopatikana kutoka katika  tendo la kutoa machozi, hiyo ndiyo maana ya kipragmatiki.

9. Tafsiri inayopatikana katika semantiki ni maana maalumu inayotolewa katika lugha WAKATI tafsiri inayopatikana katika pragmatika ni tafsiri zaidi ya lugha, kwani huhusisha hata tafsiri ya matendo mbali mbali ambayo mtu anayatenda. Mfano, maswali yafuatayo yanaweza kuulizwa katika pragmatiki (i) Ni lini tendo hilo limetendeka? Iwe ni kupitia lugha au njia nyingine yoyote (ii) Nini sababu ya kufanyika kwa tendo hilo lililotendeka?. Kwa kutafuta majibu ya maswali hayo, utakuwa unafanya tafsiri ya tendo lililotendeka, yaani tafsiri ya kipragmatiki (Recanati, 2002)

10. Kwa mujibu wa Chomsky kama jinsi alivyonukuliwa na Szabo (2005)anasema, semantiki tunaweza kuiita kuwa ni langue yaani umilisi wa lugha husika, yenye kuhusisha taratibu na kanuni zinazolinda lugha. Mfano, anavyotumia lugha kwa kufuata kanuni au muundo ulio sahihi amabapo mtu huzungumza sentensi zenye mantiki kama vile baba analima na mama anapika  WAKATIpragmatiki tunaweza kuita kuwa ni Paloe, yaani  utendaji wa mtu binafsi katika kuitumia lugha yake aliyokwisha kuwa na umilisi nayo.Mfano, mtu anavyotumia lugha kadiri ya uwezo wake mfano, mtu anaweza kusema kuwa unga unakula kuku. (Szabo, 2005)

11. Semantiki ni taaluma inayohusika na uchunguzi wa maana katika lugha itumiwayo na mwanadamu.Mfano, maana ya neno mama ikiwa na maana ya mzazi wa kikeLAKINIPragmatiki ni taalumainayohusiana na matumizi  halisi ya lugha katika muktadha tofauti  na uelewa wake kama vile malengo ya mzungumzaji na jinsi msikilizaji anavyopokea malengo hayo,Mfano, matumizi ya lugha katika muktadha wa hotelini ambapo mtu anweza kusema nipe chai tatu na akaeleweka.

12. Semantiki imegawanyika katika matawi mawili yaani semantiki ya kileksika ambayo hujihusisha na maana za maneno na mahusiano ya maana katika sentensi na tawi la pili ni semantiki ya virai au sentensi ambayo hujihusisha na maana za maneno katika kiwango cha kisintaksia WAKATI HUO Pragmatiki hujidhihirisha katika mazingira mawili yaani maana inayopatikana katika mazingira ya kiisimu. Mfano, kuna baadhi ya maneno hayawezi kupata maana mpaka yatumike na maneno mengine katika sentensi, maneno hayo kama vile na, juu ya kwa. Mfano, amekuja kwa basi. Sura ya pili ni maana inayopatikana katika matumizi yake katika muktadha fulani katika ulimwengu wa watumia lugha .Mfano, maana za maneno zitakazotumika katika muktadha wa stendi, mfano mtu anaweza kusema nitafutie vichwa vitatu na akaeleweka vizuri katika muktadha huo.

13. Katika semantiki viwango vinavyochunguzwa ni pamoja na fonimu→mofu→maneno→virai na sentensi ILI HALI Pragmatiki huchunguza zaidi namna lugha ianvyotumika katika muktadha mbalimbali. Mfano, muktadha wa buchani mtu anaweza kusema mimi utumbo na akaeleweka vizuri kabisa.


Kama unahitaji huduma ya kuandikiwa makala katika tovuti yako, au huduma yoyote basi wasiliana nami kupitia:-
SIMU:         +255 755 987 604, +255 789 198 345
E-MAIL:    reubentanzania@gmail.com



HITIMISHO
Kwa ujumla dhana hizi zinatumika sana katika ulimwengu wa watumia lugh na zinaleta ugumu katika kuzitofautisha kwani zote hujikita kuchunguza maana za maneno katika muktadha tofauti tofauti kama sehemu ya mfumo wa mazungumzo sambamba na kufafanua mfumo fungamanifu wa mazungumzo katika lugha, na hili litafanikiwa tu kwa kuzingatia maarifa ya lugha sambamba na ulimwengu halisi wa Mazungumzo.              



MAREJEO
Alghamdi, R (2013)Similarities and Differences between Semantics and Pragmatics.

Carston,R (1998) The Semantics/Pragmatics Distinction: a view from relevance theory. Katika UCL Working Papers in Linguistics.

Geoffrey Finch (2012), Linguistic; Terms and Concepts. Palgrave. Macmillan publishers

Jeffrey, C & Stanley,J (2003) Semantics, Pragmatics, and The Role of Semantic content.Oxford University Press.UK

King’ei K. (2010). Misingi Ya Isimu Jamii, Taasisi Ya Taaluma Za Kiswahili, Chuo Kikuu Dar-es-saalam.

Leech, G (1981), Semantics, Harmondswoth: Penguin books limited hazel, Watson & vinery Ltd. 

Louise McNally(1993),Semantics and Pragmatics, katika WIREs Cognitive  Science.University of Pompeu Fabra.

Masamba D.P.B. (2004). Kamusi ya isimu na falsafa ya lugha; Dare-es-Saalam.TUKI

Richmond H Thomason (2012),What is semantics? Second version:Oxford
                  UK
Recanati,F (2002)Pragmatics and Semantics.Ibis avenue de Lowendal.Paris France.
Szabo, Z.G (2005) The Distinction between Semantics and Pragmatics.Oxford University
                   Press.Oxford.
TUKI. (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Oxford University press;TUKI,  Dar-es-Saalam.
 Yule, G. (1996). Pragmatics, Oxford university press: Hong Kong.

MUINGILIANO KATI YA SEMANTIKI NA PRAGMATIKI---ACADEMICIAN BLOG

UTANGULIZI Maana ya Semantiki Richmond (2012   anafafanua maana ya Semantiki kwamba ni tawi la isimu ya lugha linalohusu viyambo ...